Jaji Luvanda ajitoa kesi ya Mbowe

Mahakamani Leo

0
202

Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi imetupilia mbali mapingamizi mawili kati ya matatu yaliyokuwa yamewasilishwa na upande wa utetezi katika kesi ya ugaidi inayowakabili Freeman Mbowe na wenzake watatu.

Uamuzi huo umetolewa na Jaji Elinaza Luvanda baada ya kupitia hoja zilizowasilishwa na upande wa jamhuri ukiongozwa na Wakili Mwandamizi Robert Kidando na ule wa Utetezi ukiongozwa na Wakili Peter Kibatala siku kadhaa zilizopita juu ya kuwepo kwa mapungufu kwenye hati ya mashitaka.

Mapingamizi hayo yalikuwa ni pamoja na mashitaka mawili yanayofanana kuwekwa katika hati ya mashitaka moja ambapo shitaka la kula njama kujumuishwa na shitaka la kushiriki vikao vya kigaidi kwamba haikupaswa kuwepo kwenye shitaka la kula njama.

Pingamizi lingine ni kuhusu sheria ya ugaidi ambayo washitakiwa wanashtakiwa nayo kwamba haifafanua viambato vya kosa la ugaidi.

Mahakama imejiridhisha na shitaka la kwanza, la nne na sita kuwa yalikuwa na mapungufu ya kisheria hivyo kutoa maelekezo kwa mawakili wa upande wa jamhuri kufanya marekebisho ya mashitaka hayo.

Pia imeahirisha kutoa uamuzi wa pingamizi la kwanza linalohusu upungufu wa sheria ya ugaidi kutokueleza malengo ya vitendo vya ugaidi baada ya kushindwa kupata kwa haraka kumbukumbuku za bunge (Hansard) ili kufanya utafiti zaidi kujua lengo la bunge lilikuwa nini wakati wa kutunga sheria zinazohusu kesi za ugaidi kwa kuwa kuna baadhi ya maneno yaliachwa tofauti na mwongozo wa kimataifa juu ya utungaji wa sheria za ugaidi duniani.

“Bunge halikuchagua mlango wa kutoa tafsri ya ugaidi hivyo haitoshi kusema kwamba sheria zetu zinafanana na sheria za wenzetu hivyo ni vyema kwenda mbali zaidi,” amesisitiza Jaji Elinaza Luvanda.

Baada ya uamuzi huo mshitakiwa Freeman Mbowe alimwomba Jaji Luvanda kujitoa kwenye kesi hiyo kwa kile alichoeleza kuwa kukosa imani nae katika kufanya rejea kwenye baadhi ya kesi zilizowasilishwa na mawakili wao, ikiwemo kuahirisha kufanya uamuzi wa moja ya pingamizi na kutozingatia pingamizi lililopita juu ya mamlaka ya mahakama hivyo kuwafanya washitakiwa kuona hawatatendewi haki.

Aidha mshitakiwa Mbowe ameeleza mahakama hiyo kuwa kesi hiyo inavuta hisia ndani jamii kwa mujibu na mtandao wa Wilkileaks hivyo kuomba kesi hiyo iendeshwe pasi kufuata hisia ambazo anadaiwa .

Jaji Luvanda amekubali kujitoa kwenye shauri hilo kwa kudai kuwa ombi la mshitakiwa Mbowe ni la msingi na lina maslahi mapana kwa umma licha ya kuwa malalamiko hayo ni yakudhani hivyo kuomba kukaa pembeni.

Kesi hiyo imahirishwa mpaka pale mahakama itakapopanga jaji mwingine atakayendelea na shauri hilo, na washitakiwa wamerudishwa Rumande.