Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Stephen Kagaigai amesema kuna uhitaji miradi inayotekelezwa mikoani kusimamiwa kwa ngazi ya mkoa husika badala ya serikali kuu ili kuharakisha ukamilishaji wa miradi hiyo.
Kagaigai ameyasema hayo wakati akizungumza na TBC, na kuongeza kuwa ujenzi wa miradi ya jengo la mama na mtoto pamoja na jengo la huduma za dharura katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mawenzi umekuwa wa kusuasua kutokana na ucheleweshwaji wa fedha kutoka wizarani.
Kagaigai amesema kwa kipindi cha takribani miaka 12 sasa jengo la mama na mtoto halijakamilika na akihoji a anaambiwa fedha kutoka wizarani bado hazijafika.
“Yani inasikitisha miaka 12 jengo bado linajengwa huku akina mama wajawazito wanaendelea kuteseka kwa kukosa huduma mbalimbali ikiwemo kliniki ya mama na mtoto,” amesema Kagaigai
Katika hatua nyingine, Kagaigai amemuagiza Katibu Tawala Mkoa Dkt. Seif Shekalaghe kufuatilia wizara ya fedha ili waweze kutoa fedha za kumalizia ujenzi wa mradi wa stendi ya kimataifa ya Ngangamfumuni ambao kwa sasa umesimama.
Akitolea ufafanuzi suala la ujenzi wa stendi ya Ngangamfumuni, Shekalaghe amesema tayari ameshafuatilia wizara ya fedha ili waweze kupatiwa shilingi bilioni 10 za kumaliza awamu ya kwanza ya ujenzi huo.