Watendaji wa kata 16 Same wakabidhiwa pikipiki

0
141

Halmashauri ya wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro imetumia shilingi milioni 37.6 zilizobaki baada ya kununua gari la Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, kununua pikipiki 16 kwa ajili ya watendaji wa kata ili waweze kuzitumia kukusanya mapato.

Akizungumzia hatua hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Same, Annastazia Tutuba amesema katika mwaka wa fedha wa 2020/2021 walipokea kutoka hazina shilingi milioni 210, ambapo walinunua gari la Mkurugenzi kwa shilingi milioni 162.

Amesema baada ya fedha kubaki, waliomba kibali hazina cha kununua pikipiki hizo, ili Watendaji wa kata hasa zilizoko milimani ambapo kuna changamoto ya usafiri waweze kuzitumia kukusanya mapato ya Serikali bila usumbufu.

“Zipo kata zilizoko katika maeneo ya milimani hakuna hata usafiri wa umma, hivyo pikipiki hizo zitawasaidia Watendaji hao kukabiliana na adha hiyo hasa maeneo yenye miundombinu mibovu ya barabara.”amesema Tutuba.

Akikabidhi pikipiki kwa Watendaji 16 wa baadhi ya kata za wilaya hiyo, Mkuu wa wilaya ya Same, Edward Mpogolo amesema hatua hiyo itasaidia kurahisisha Watendaji kutekeleza majukumu yao katika kusimamia vema ukusanyaji wa mapato katika kata zao, na kwamba hatua kali zitachukuliwa kwa atakayetumia usafiri huo kinyume na utaratibu.

Nao baadhi ya Watendaji waliokabidhiwa pikipiki hizo wamesema zitawasaidia kuondokana na changamoto ya kutumia gharama kubwa kwa kukodisha usafiri binafsi pindi wanapoenda kukusanya mapato katika maeneo yao.