Shughuli za usafirishaji kati ya Stesheni ya Manyoni, Itigi na mikoa ya Kanda ya ziwa zimesimama kwa muda baada ya eneo la ardhi kutitia na kutengeneza shimo kando ya reli nje kidogo ya mji wa Itigi mkoani Singida.
Baadhi ya wakazi wa kijiji cha Kitopeni wamesema walisikia kishindo kikubwa wakati mvua ikinyesha kilichosababisha nyufa na mashimo katika baadhi ya maeneo ambapo pia nyumba tatu zimebomoka.
Hali hiyo imeathiri shughuli za usafirishaji reli ya kati baina ya stesheni ya Itigi na Manyoni na hivyo kusababisha kukatika kwa mawasiliano kati ya Singida na mikoa ya Kanda ya ziwa inayotumia usafiri huo wa reli.
Tayari mafundi wa kampuni ya Reli Tanzania wamefika katika eneo hilo kuanza ukarabati wa eneo la reli lililoharibika ili kurejesha huduma za usafiri.
Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa wa Singida wametembelea maeneo yaliyoathirika na mvua hiyo ambapo Mwenyekiti wa Kamati hiyo Dkt. Rehema Nchimbi amesihi wananchi kuwa watulivu wakati serikali inatafuta mtaalamu wa miamba kufanya uchunguzi wa kina katika maeneo hayo yaliyotitia.