Prof. Ole Gabriel : Dkt. Kikwete alinijengea msingi

0
115

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Profesa Elisante Ole Gabriel amesema anamshukuru Rais mstaafu wa awamu ya nne Dkt. Jakaya Kikwete kwa kuwa ndiye aliyemuibua katika uongozi mwaka 2013 kwa kumteua kwa mara ya kwanza kuwa Naibu Katibu Mkuu wa wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Profesa Ole Gabriel amebainisha hayo jijini Dodoma wakati akizungumza na menejimeti ya wizara ya Mifugo na Uvuvi katika ofisi za wizara hiyo alipofika kwa ajili ya kukabidhi ofisi aliyokuwa akihudumu kama Katibu Mkuu anayeshughulikia Mifugo.

Aidha Profesa Ole Gabriel amebainisha kuwa siku chache kabla ya Dkt. Kikwete kuondoka madarakani mwezi Oktoba mwaka 2015, alimteua kuwa Katibu Mkuu wa wizara ya Habari, Utamadani, Sanaa na Michezo, hivyo hana budi kumshukuru kwa kuwa alionesha imani kubwa kwake.

Pia, amesema anashukuru aliendelea kuaminiwa na Rais wa awamu ya Tano Hayati Dkt.John Magufuli ambaye alimteua kushika nafasi ya Katibu Mkuu wizara tofauti na Rais wa awamu ya sita Samia Suluhu Hassan ambaye alimteua kuwa Katibu Mkuu wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo nafasi ambayo amehudumu hadi alipoteuliwa kuwa Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania.

“Namshukuru sana Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwa na imani nami katika nafasi hii mpya aliyoniteua ya kuwa Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, na kwamba nitafanya kazi kwa nguvu na weledi mkubwa kwa kushirikiana na wenzangu kwa kuwa nina deni kubwa la kulipa kwa Rais Samia, lakini pia kufikia matarajio ya Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahim Juma na matarajio ya Watanzania wote katika mhimili huu kwenye utendaji wa haki.” Amesema Profesa Gabriel

Katika hatua nyingine, Mtendaji Mkuu huyo wa Mahakama ya Tanzania Profesa Elisante Ole Gabriel amefanya mazungumzo na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mashimba Ndaki katika ofisi za wizara hiyo ambapo Waziri Ndaki amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwa na imani kubwa na Profesa Ole Gabriel kwa kumteua kuwa Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania kutoka katika nafasi aliyokuwa akihudumu ya Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo.