Kiwanda chatakiwa kutenga eneo la kuhifadhi bidhaa za chakula

0
160

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Selemani Jafo, ametoa muda wa miezi sita kwa wamiliki wa kiwanda cha Matson Group kinachozalisha bidhaa za plastiki, rangi na chuma kuhakikisha wanatenga eneo maalum la kuhifadhi bidhaa za chakula, ili kuepusha athari za kiafya kwa Wananchi.

Waziri Jafo ametoa agizo hilo mkoani Dar es Salaam baada ya kukagua viwanda vya Kiboko na Sayona pamoja na kiwanda cha kuzalisha bidhaa za plastiki zilizo chini ya Maston group, na kubaini kuwepo kwa shehena ya kuhifadhi vinywaji kwenye eneo hatarishi.

Katika hatua nyingine Waziri Jafo amekataa kusaini kibali cha ukusanyaji wa chuma chakavu cha Iron steel, mpaka hapo uongozi wa kiwanda hicho utakaporekebisha mtambo wa kutolea Moshi kiwandani hapo.

Aidha amewaonya Viongozi wa kiwanda hicho kuacha tabia ya kutumia fedha kuwanunua viongozi wa Serikali, ili wasitekeleze wajibu wao kwa mujibu wa sheria

Katika Ziara hiyo pia Waziri Jafo ameeleza kuridhishwa na mfumo wa maji taka wa kiwanda cha Cocacola kwanza na kuwataka wawekezaji wengine kuiga mfano wa kiwanda hicho kama sehemu ya kudhibiti athari za kimazingira.