Kaya 19 katika kitongoji cha Shaurimoyo wilayani Rufiji mkoani Pwani hazina mahali pa kuishi, baada ya nyumba zao kuteketea kwa moto usiku wa kuamkia leo.
Baadhi ya Wakazi wa kitongoji hicho wamedai chanzo cha moto huo ni mwenzao mmoja aliyekuwa akisafisha eneo lake kwa moto, ambaye baadaye alishindwa kuudhibiti.
Wamesema mali zote zilizokuwemo ndani ya nyumba hizo 19 zimeteketea kabisa na moto, lakini hakuna mtu aliyejeruhiwa.
Kufuatia tukio hilo, Mkuu wa mkoa wa Pwani ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Abubakar Kunenge akiwa pamoja na wajumbe wa kamati hiyo wamefika katika kitongoji hicho cha Shaurimoyo kuangalia athari zilizosababishwa na moto huo pamoja na hatua zilizochukuliwa kuwasaidia waathirika.
Amewapongeza wakazi wa maeneo ya karibu kwa kuwapatia hifadhi Wananchi wenzao ambao nyumba zao zimeteketea kwa moto.
Kunenge ameuagiza uongozi wa wilaya ya Rufiji kufanya tathmini haraka iwezekanavyo, ili kujua athari iliyotokana na moto huo.