Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani amewataka wakazi wa mikoa ya Iringa na Njombe kutumia fursa ya uwepo wa viwanda vya kuzalisha nguzo za umeme kwenye maeneo yao kwa kupanda miti ya kutosha kwa kuwa soko lipo.
Dkt. Kalemani ametoa kauli hiyo kwenye hafla ya uzinduzi wa kiwanda cha kuzalisha nguzo cha Qwihaya, kijiji cha Mtwango wilayani Njombe.
Kiwanda hicho chenye uwezo wa kuzalisha nguzo 1,500 kwa siku ni cha pili kwa kampuni hiyo baada ya kile cha Mufindi, Iringa huku vyote vikitoa ajira kwa wakazi zaidi ya 800 katika mikoa hiyo.
Waziri Kalemani amevitaka viwanda vya kuzalisha nguzo za umeme nchini kuzingatia viwango vya ubora ili serikali isiagize nguzo hizo nje ya nchi.
Kwa kutambua mchango wa serikali kwenye wawekezaji, Mkurugenzi wa Kampuni ya Qwihaya, Leonard Mahenda ameahidi kugharamia uunganishaji wa umeme katika shule za msingi na sekondari za wilaya za Njombe na Ludewa.