Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango ameiomba Serikali ya Italia kuendelea kuwekeza zaidi katika elimu ya ufundi nchini, kwa kuwa elimu hiyo imekua na mchango mkubwa katika maendeleo ya Taifa.
Makamu wa Rais ametoa ombi hilo Ikulu jijini Dar es Salaam alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Italia hapa nchini, Marco Lambardi.
Amesema Serikali ya Tanzania inatambua mchango mkubwa wa Serikali ya Italia katika kuendeleza elimu ya ufundi hapa nchini, kwa kuwa umesaidia watu wengi kupata elimu hiyo hasa vijana.
Katika mazungumzo hayo, Makamu wa Rais Dkt. Mpango amemhakikishia balozi huyo wa Italia hapa nchini kuwa Tanzania itaendelea kuimarisha ushirikiano uliopo baina ya nchi hizo mbili katika nyanja mbalimbali za maendeleo.
Kwa upande wake Balozi Marco Lambardi amesema Italia na Tanzania zimekua na ushirikiano wa muda mrefu, hivyo wataendelea kuwekeza nchini katika sekta mbalimbali ikiwemo kilimo na viwanda.
Amesema tayari wapo katika kufanya makubaliano ya kuanzisha safari za ndege za moja kwa moja kutoka Italia hadi Zanzibar, ili kuendelea kukuza sekta ya utalii hapa nchini.