Na Happyness Simon Hans
Mtu mmoja ameuawa kwa kupigwa risasi katika moja ya geti ya kuingilia katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kabul nchini Afghanistan.
Mbali na kifo hicho, watu wengine watatu wamejeruhiwa katika tukio hilo lililotokea mapema hii leo, ambapo mamia ya raia wa Afghanistan wameendelea kufika katika uwanja huo wa ndege kutafuta usafiri wa kuondoka nchini humo baada ya kundi la wapiganaji wa Taliban kutwaa uongozi wa Taifa hilo.
Katika hatua nyingine zoezi la kuwaondoa raia wa kigeni pamoja na wale wa Afghanistan limeendelea kufanyika, ambapo hii leo Ubelgiji imetuma ndege ya kuwaondoa raia takribani 193 na kuwapeleka kuwapatia hifadhi ya muda katika eneo la jirani na kambi ya jeshi la anga la nchi hiyo katika mji wa Brussels.
Naye Rais Joe Biden wa Marekani amesema nchi yake inafanya jitihada za kuongeza idadi ya ndege ili kuweza kuwaondoa watu wengi zaidi wanaofika katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kabul kutafuta usafiri kuondoka nchini humo.
Amesema tayari Marekani imewaondoa watu elfu 28 kutoka nchini humo, na kuongeza kuwa idadi hiyo inaweza kuongezeka.