Mpango wa Elimu Haina Mwisho warejesha ndoto za wanafunzi

0
147

Mpango wa Elimu Haina Mwisho huo unaoendeshwa katika takribani vyuo 54 kwa upande wa Tanzania Bara umewanufaisha watoto wa kike waliokatisha masomo kutokana na changamoto za ujauzito na uwezo duni wa kiuchumi katika familia zao.

Mmoja wa wanufaika wa mpango huo Judith Mwadisa anayesoma katika Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Katumba kilichopo wilayani Rungwe mkoani Mbeya amesema alikatisha masomo baada ya wazazi wake kufariki.

Anasema baada ya kuona fursa ya masomo ya elimu haina mwisho alijiunga na chuo hicho ambapo kwa sasa anaendelea na masomo ya kidato cha pili sambamba na mafunzo ya ufundi wa umeme majumbani.

Naye Maria Kajuni aliyeacha shule kidato cha tatu baada ya kupata ujauzito ametumia fursa ya kujiunga na chuo hicho ambapo anasoma kidato cha pili, anapata mafunzo ya ushonaji huku mwanaye akihudumiwa chuoni hapo kwa elimu ya makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto.

Baadhi ya wazazi wa watoto hao wameishukuru serikali kwa kutoa fursa hiyo kwa watoto wao wa kike iliyorejesha ndoto za mabinti zao.

Mkuu wa chuo, Musa Mturuki amesema uwekezaji uliofanywa na serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia wa shilingi milioni 686 za maboresho ya mabweni, karakana na miundombinu ya chuo umekuwa chachu kubwa ya kuongeza udahili wa wanafunzi.