Mwanafunzi Oscar Herman wa kidato cha sita katika shule ya sekondari ya ufundi Ifunda amebuni kifaa maalum ambacho kitasaidia kupunguza madhara yatokanayo na majanga ya moto shuleni
Oscar anasema kifaa hicho kinaunganishwa na mfumo wa umeme ambapo inapotokea hitilafu ya umeme hutoa taarifa kwa mlio wa sauti pamoja na ishara kupitia mtambo maalum unaowekwa katika ofisi ya mkuu wa shule.
Oscar anasema alipata wazo hilo baada ya kuona tabia za wanafunzi kujiunganishia vifaa vya umeme mabwenini na kuhatarisha usalama wao.
Aidha ubunifu wake tayari umesajiliwa katika mamlaka husika na umefanyiwa majaribio katika baadhi ya mabweni shuleni hapo.
Katika hatua nyingine kijana Isaya William wa kidato cha kwanza amebuni roboti ya kupulizia dawa katika mashamba.
Roboti hiyo itakayoendeshwa kwa mfumo unaounganishwa na simu, itamfanya mkulima kupuliza dawa akiwa nyumbani, kuepuka madhara ya dawa hizo pamoja na kuokoa muda wa utendaji kazi.
Mkuu wa shule ya sekondari ya ufundi Ifunda Yusuph Mugala amesema shule hiyo inawaendeleza vijana wabunifu ili walete tija kwa taifa.