Waziri aagiza Askofu Gwajima kukamatwa

0
664

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima ameagiza kukamatwa kwa mbunge wa jimbo la Kawe, Askofu Josephat Gwajima kwa madai ya kuwa anaivuruga wizara yake na serikali kwa ujumla hasa katika mapambano dhidi ya UVIKO-19.

Dkt. Gwajima ametoa agizo hilo wilayani Butiama mkoani Mara ambapo amesema kwa muda mrefu sasa Askofu Gwajima amekuwa akitoa kauli za kupotosha kuhusiana na chanjo ya ugonjwa huo jambo ambalo limekuwa likiivuruga serikali.

Amesema Gwajima amekuwa akitumia kanisa lake na kujifanya kuwa msemaji na mtetezi wa wananchi huku akitoa taarifa za uongo ikiwemo tuhuma dhidi ya waziri wa afya pamoja na Rais Samia Suluhu Hassan kuwa walipewa rushwa ili kuruhusu chanjo ianze kutolewa nchini.

Waziri amesema mara kadhaa Gwajima amekuwa akitoa taarifa za kupotosha juu ya chanjo na hakuna hatua zinazochukuliwa dhidi yake jambo ambalo limekuwa likileta mkanganyiko katika jamii na kwamba sasa umefika mwisho wa upotoshaji huo

Amesema kuwa sekta ya afya sio ya kuchezewa hivyo yeyote atakayejaribu kupotosha au kuvuruga mipango ya serikali kupitia sekta hiyo lazima hatua kali zitachukuliwa bila kujali nafasi yake au uhusiano wake na mtu yeyote.

Askofu Gwajima anatakiwa kutoa uthibitusho wa kisayansi juu ya madai yake hayo la sivyo hatua za kisheria lazima zichukuliwe.

Waziri amesema Serikali haimuogopi mtu yeyote bali inafanya kazi kwa mujibu wa sheria na kabla ya serikali kuanza kuruhusu Watanzania kuchanjwa utafiti ulifanyika ili kujua usalama wa chanjo hiyo.