Waziri Mkuu aagiza vigogo Manispaa ya Temeke kufikishwa Mahakamani

0
191

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema hajaridhishwa na gharama za ujenzi wa miradi ya barabara ya Kijichi–Mwanamtoti yenye urefu wa kilomita 1.8 iliyogharimu shilingi bilioni 5.4 na barabara ya Kijichi-Toangoma yenye urefu wa kilomita 3.25 iliyogharimu shilingi bilioni 13.5.

Waziri Mkuu Majaliwa ametoa ameyasema hayo wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua miradi ya ujenzi wa barabara za Kijichi-Mwanamtoti na Kijichi-Toangoma wilayani Temeke na kituo cha Mabasi kilichopo Buza. Miradi hiyo inajengwa kupitia mradi uendelezaji wa Jiji la Dar es Salaam (DMDP).

Kufuatia hatua hiyo, Waziri Mkuu Majaliwa ameiagiza Taasisi za Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ihakikishe watu wote waliohusika na ubadhilifu huo wa fedha ambao tayari walishasimamishwa kazi wawe wamefikishwa mahakamani kabla ya Agosti 20, 2021.

Halikadhalika, Waziri Mkuu Majaliwa ametumia fursa hiyo kumtaka Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke Elihuruma Mabelya ahakikishe anasimamia na anazingatia maslahi ya Wana-Temeke katika utekelezaji wa majukumu yake.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu Majaliwa ameiagiza TAKUKURU iwatafute viongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke waliohusika katika kukopa shilingi bilioni 19 kwa ajili ya ulipaji fidia ya ujenzi wa miradi mbalimbali warudishwe ili ajibu tuhuma zinazowakabili.

Mbali na agizo hilo, pia Waziri Mkuu Majaliwa ameelekeza kusimamishwa kwa mradi wa ujenzi wa kituo cha mabasi Buza hadi hapo Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Ummy Mwalimu atakapojiridhisha ni mradi gani unapaswa kufanyika katika eneo hilo.

Akizungumzia kuhusu eneo la Temeke Kota, Waziri Mkuu Majaliwa ameuagiza uongozi wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) na uongozi wa Manispaa ya Temeke wakutane na wafanye uamuzi juu ya matumizi ya eneo hilo na baada ya wiki moja wampelekee taarifa ya walichopanga kukifanya.