Shilingi bilioni 985 kuboresha vyuo vikuu vya Umma

0
221

Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi unaogharimu dola za kimarekani milioni 425 ambazo ni sawa na shilingi bilioni 985 unatarajiwa kuanza mwaka huu wa fedha.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa James Mdoe amesema hayo katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Mkwawa ambacho ni sehemu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alipokuwa akizungumza kuhusu mafanikio ya serikali kwenye elimu ya Juu.

Amesema mradi huo wa miaka mitano unaoanzia mwaka huu wa fedha, utatekelezwa kwenye vyuo vikuu vyote vya umma pamoja na vyuo vishiriki.

Vile vile utatekelezwa na Tume ya Vyuo Vikuu (TCU), Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HELSB) pamoja na Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech).

Ameema lengo la mradi huo ni kuzalisha wahitimu wenye taaluma ya stadi stahiki ili kukidhi mahitaji ya soko la ajira na kusaidia katika mageuzi ya viwanda kwa sababu ndani ya mradi kuna sehemu kubwa ya kusomesha wahadhiri wakiwemo wale wanaoenda kusoma upya na wale wanaoendelea na kazi kupata mafunzo kazini.