Jeshi la Polisi nchini limesema uhalifu nchini umepungua kwa kiasi kikubwa jambo ambalo limefanya hali ya usalama kuwa ya kiwango cha juu.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Inspekta Jenerali Simon Sirro jijini Dar Es Salaam kwenye hafla ya kuwatunuku wahitimu waliofanya vizuri katika mafunzo ya uofisa na ukaguzi wa jeshi la polisi.
Amesema hali ya mwaka huu imekuwa tofauti katika usalama.
“Kiwango cha uhalifu kimepungua kwa kiasi kikubwa na hii imetokana na ushrikiano mkubwa wa wananchi, polisi na vyombo vya usalama hapa nchini jambo linaloashiria alama nzuri ya ushirikiano hapa nchini”alisema IGP Sirro.
Kamanda Sirro amesema uhalifu katika makosa ya unyang’anyi umepungua kwa asilimia 25, uhalifu wa makosa ya usalama barabarani ukiwa umepungua kwa asilimia 32.
Katika hatua nyingine Kamanda Sirro amesema kwa mwaka huu jeshi la polisi kupitia makosa ya barabarani limeingiza mapato ya shilingi Bilioni 63.8 ikilinganishwa na mwaka jana ambapo mapato yalikuwa shilingi Bilioni 62.2.