Wakati baadhi ya watu wakidai kuwa hawataki kuchoma chanjo ya UVIKO-19 kwa hofu kuwa watapata tatizo la damu kuganda, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, Prof. Mohamed Janabi ameeleza kuwa watu wasiochanjwa ndio wapo hatarini zaidi kupata tatizo hilo.
Prof. Janabi amefafanua hilo katika mahojiano maalum na TBC na kueleza kuwa kati ya watu 1,000,000 waliopata chanjo, ni wanne tu, sawa na asilimia 0.0004 ndio wanapata tatizo la damu kuganda, wakati kati ya watu 1,000,000 wanaopata maambukizi ya UVIKO-19 ambao hawajachanjwa, watu 165,000 sawa na asilimia 16.5, wanapata tatizo hilo na ndilo linalosababisha vifo.
Aidha, amesema wakati watu wakiwa na hofu ya chanjo, kuna mambo mengine yanayosababisha damu kuganda kama vile uvutaji wa sigara ambapo kati ya watu 1,000,000 wanaovuta, 1,763, sawa na asilimia 0.18 hupata tatizo hilo, huku kati ya watu 1,000,000 wanaotumia vidonge vya uzazi wa mpango, 500-1,200 sawa na asilimia 0.05 hadi 0.12 hupata tatizo la kuganda damu.
“Nasisitiza, chance [uwezekano] ya wewe kupata damu kuganda ni kubwa zaidi ukiwa na ugonjwa [UVIKO-19] kuliko hiyo ‘chance’ ya kwenye chanjo,” ameeleza Prof. Janabi, na kuongeza kuwa kuna utaratibu wa kutibu mtu anapopata tatizo hilo.
Aidha, ameeleza kuwa mwongozo wa Shirika la Afya Duniani (WHO) halizuii mama mjamzito kupata chanjo kwa sababu haina madhara. Pia amewataka vijana kutokudhani kuwa hawawezi kupata maambukizi, hivyo ni vyema wakajitokeza kupata chanjo baada ya serikali kuruhusu wote kuchanjwa kuanzia miaka 18.
Prof. Janabi ameendelea kusisitiza Watanzania kuwa chanjo ni salama na kwamba baada ya chanjo ya Johnson & Johnson kuletwa nchini, watalaamu walitumia siku kadhaa kuhakiki usalama wake na wakajiridhisha kuwa zinafaa kutumika.