Mradi wa umeme jadidifu kuipaisha Tanzania

0
215

Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, imewekeza zaidi ya shilingi bilioni 37.4 katika uanzishwaji wa wa kituo cha kipekee cha umahiri cha kikanda katika nishati jadidifu (EASTRIP) katika Chuo Cha Ufundi Arusha eneo la Kikuletwa wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro.

Kaimu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Ufundi Arusha Dkt. Yusuph Mhando, amesema kituo hicho kinachotarajia kukamilika mwaka 2025 kitakuwa kitovu cha mafunzo ya vitendo kwa wataalam mbalimbali wa nishati ya umeme.

Amesema kituo hicho kitatumika kutoa wataalam mbalimbali wa fani ya nishati watakaotumika kuendesha miradi mikubwa ya kitaifa ikiwemo mradi wa umeme wa maji wa Julius Nyerere pamoja na ile inayotekelezwa na Shirika la Umeme Tanzania-TANESCO.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya mradi huo Dkt. Erick Mgaya amesema watazalisha umeme wa megawati 1.65 kwa kutumia nishati jadidifu ikiwemo vyanzo vya maporomoko ya maji, jua, upepo na takangumu.
Mradi huo unatarajia kuwa kituo cha kipekee cha utafiti wa nishati jadidifu na kuiunganisha Tanzania na Mataifa ya Ukanda wa Afrika Mashariki.