Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) yaongeza muda wa kuhifadhi makontena bandarini kutoka siku saba kwa makontena tupu hadi siku 21 na siku saba kwa makontena yenye mizigo hadi siku 14 kwa mikoa yatakayotumia bandari ya Mtwara.
Uamuzi huo umefikiwa kufuatia agizo la Rais, Samia Suluhu Hassan kuitaka TPA kutumia bandari ya Mtwara kusafirisha korosho zinazozalishwa kwenye mikoa hiyo mitatu.
Meneja wa bandari ya Mtwara Mhandisi Juma Kijavara amesema bandari hiyo inatarajia kusafirisha tani zaidi ya 250,000 za korosho kutoka katika mikoa hiyo kati ya tani 280,000 zinazotarajiwa kuzalishwa katika mikoa hiyo kwa msimu wa mwaka 2021/2022.
Pamoja na mikakati mingine ambayo imewekwa na bandari ya Mtwara, kwa sasa bandari hiyo ina uwezo wa kuhudumia meli nne zenye urefu wa mita 150 kwa wakati mmoja kutoka meli mbili hapo awali.
Akifungua semina iliyotolewa kwa waandishi wa habari kuhusu mkakati wa bandari hiyo na manufaa yake kwa jamii, Katibu Tawala wa wilaya ya Mtwara, Thomasi Salala amewataka waandishi kutumia vema kalamu zao katika kuitangaza bandari ya Mtwara kuelekea msimu wa korosho wa mwaka 2021/2022.
Kwa upande wao baadhi ya waandishi wa habari waliopatiwa mafunzo hayo wamesema yatawaletea tija katika kuhabarisha wananchi mambo kadha wa kadha yanayofanywa na bandari hiyo.
Bandari ya Mtwara kwa sasa imeongeza uwezo wa kuhudumia tani laki nne kwa mwaka hadi kufikia tani milioni moja kwa mwaka, hii inatokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na serikali katika bandari ya Mtwara.