Mradi wa maji Mlandizi Mboga wakamilika 95%

Chalinze, Pwani

0
223

Wakazi wa Halmashauri ya Chalinze Mkoani Pwani wamesema matumizi ya maji ya rambo na visima itabaki kuwa historia baada ya mradi wa maji Mlandizi Mboga kukamilika Asilimia 95.

Kiongozi wa Mbio za Mwenge kitaifa Luteni Josephine Mwambashi amezuru kwenye mradi huo na kuridhishwa na Maendeleo yake huku akiagiza Wasimamizi wa Miradi yote ya Maendeleo kushirikisha wananchi wa maeneo husika.

Luteni Mwambashi amesema fedha zilizotumika kwenye mradi umeendana na thamani ya ubora wa mradi huo na kupongeza uongozi wa DAWASA kwa usimamizi bora wa fedha.

Wakizungumza baada ya kuzinduliwa kwa Mradi huo wakazi wa Chalinze wamesema kwa Muda mrefu wamekuwa wakitumia Maji ya Rambo ambayo si salama kwa Afya zao huku watoto wa shule wakitembea umbali mrefu kufuata maji.

Wamesema kukamilika kwa mradi huo utaleta fursa za ajira kupitia uwazishaji wa viwanda mkoani humo.

Kwa Upande wake mtendaji Mkuu wa DAWASA Mhandisi Cyprian Luhemeja amesema mradi huo umefikia asilimia 95 huku ikitarajia kuhudumia wateja zaidi ya Laki Moja.

Mhandisi Luhemeja amesema kati ya Bilioni 17 zilizotolewa kwa ajili ya Mradi huo mpaka sasa zimeshatumika Bilioni 13 tu.

Mradi wa maji Mlandizi Mboga unatarajia kuanza kusukuma Maji kwa Wananchi Mwishoni mwa Mwezi Septemba Mwaka huu.