Pato la Taifa kwa kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka 2021 limeongezeka hadi shilingi trilioni 38.0 kutoka shilingi trilioni 36.4 katika kipindi kama hicho kwa mwaka 2020.
Hayo yamesemwa na Kaimu Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Daniel Masolwa jijini Dodoma wakati wa mkutano na waandishi wa habari uliolenga kueleza hali ya ukuaji wa uchumi.
“Katika kipindi cha robo ya kwanza 2021, shughuli za uchimbaji madini na mawe zimeongoza kwa kuwa na kiwango cha juu zaidi cha ukuaji wa asilimia 10.2, ikifuatiwa na habari na mawasiliano asilimia 9.1, uchukuzi na uhifadhi mizigo 9.0, maji safi na majitaka 9.0, huduma za kitaalam, sayansi na ufundi 7.8, huduma zinazohusiana na utawala asilimia 7.4 na umeme 7.2,” amesisitiza Masolwa
Kwa mujibu wa Sheria ya Takwimu Sura 351, takwimu hizi za Pato la Taifa kwa robo ya kwanza ya mwaka 2021 ni rasmi na zinatumika katika kufuatilia na kutathmini malengo yaliyowekwa katika sekta za kiuchumi.