Serikali yaanza kusaka matokeo chanya ya zao la mwani

0
227

Serikali imesema itaendelea kuwawezesha wakulima wa zao la mwani kwa vifaa pamoja na utaalamu ili waweze kuzalisha kwa wingi na ubora unaohitajika sokoni.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki amesema hayo akiwa katika Kijiji cha Zingibari kilichopo Wilaya ya Mkinga mkoani Tanga, wakati akitoa vifaa vyenye thamani ya shilingi milioni 4 kwa ajili ya kilimo cha mwani kwa vikundi vitatu vya wakulima.

“Huu msaada wa vifaa kwa ajili ya kilimo utafika katika maeneo yote yenye uzalishaji na msisitizo tumeanza kuweka kwenye elimu ya namna ya kulima zao la mwani kwa ajili ya tija zaidi,” amesema Waziri Ndaki

Aidha, akiwa katika Kata ya Kipumbwi wilaya ya Pangani amesema serikali inatarajia kutumia shilingi bilioni 1.2 kwa ajili ya ujenzi wa soko la kimataifa katika kata hiyo kwa ajili ya kuuza dagaa ndani na nje ya nchi.

Ndaki amesema wanunuzi wa dagaa wanaotoka nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Zambia, Malawi, Rwanda na Burundi wataenda kununua dagaa kutoka Kipumbwi hivyo wafanyabiashara wa kata hiyo hawatapata shida ya kutafuta soko la dagaa.