Wiki ya AZAKI yazinduliwa Dar

0
202

Msajili wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali (NGOs), Vickness Mayao amezindua rasmi wiki ya Asasi za Kiraia (AZAKI) inayotarajiwa kufanyika Oktoba 25 hadi Oktoba 29 mwaka huu huku akitumia nafasi hiyo kuwapongeza viongozi wapya wa Baraza la Kitaifa la Mashirika yasiyo ya Kiserikali kupitia Mwenyekiti na timu yake yote.

Akizungumza wakati akizindua wiki hiyo ,Mayao amesema hiyo ni mara yake ya pili kupata nafasi ya kukutana na wakuregenzi wa asasi za kiraia nchini pamoja na wadau wengine wa maendeleo, baada ya mkutano wa kikao kazi uliofanyika Januari mwaka huu.

“Ama kwa hakika fursa hizi za kukutana nanyi zimeendelea kuwezesha uimarikaji wa mahusiano na mashirikiano kati ya asasi za kiraia na Serikali kupitia Ofisi ya Msajili na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini. Nichukue nafasi hii kutoa pongezi za dhati kwa mara nyingine tena kwa uongozi mpya wa Baraza la Kitaifa la Mashirika yasiyo ya Kiserikali, kupitia Mwenyekiti na timu yake yote.

“Wizara Pamoja na ofisi yangu tulipata faraja kubwa kuona kuwa sasa uongozi na uratibu wa sekta ya asasi za kiraia nchini umerejea mahali pake. Sote ni mashahidi wa madhara yaliyojitokeza kutokana na ukosefu wa uongozi na uratibu wa sekta ya asasi za kiraia nchini kwa miaka kadhaa.Nipende kuwaahidi kuwa ofisini yangu iko tayari kushirikiana nanyi kwa karibu sana kuhakikisha ustawi na usimamizi dhabiti wa sekta ya asasi za kiraia nchini,”amesema Mayao.

Aidha ametoa pongezi kwa kamati ya uchaguzi wa NaCoNGO chini ya Mwenyekiti wake Flaviana Charles wakili msomi na uratibu makini wa mchakato mzima kupitia Mkurugenzi wa Foundation for Civil Society Francis Kiwanga.”Hakika mmedhihirisha bayana nguvu ya umoja na mshikamano ambayo ikiendelea kutumika vizuri itapelekea mapinduzi na maendeleo ya hali ya juu kwa sekta hii ya Asasi za kiraia nchini.”