Benki Kuu yaleta neema ya mikopo

0
356

Tanzania ikiendelea kukabiliana na janga la Virusi vya Korona (UVIKO19), Benki Kuu ya Tanzania (BoT) nayo imechukua hatua zaidi ambapo imeanzisha mfuko utakaowezesha wananchi kupata mikopo kwa riba isyozidi asilimia 10 kwa mwaka.

Gavana wa BoT, Prof. Florens Luoga amesema kuwa wameanzisha mfuko maalumu wenye thamani ya shilingi trilioni 1 kwa ajili ya kuzikopesha benki taasisi za fedha kwa riba ya asilimia tatu, ili nazo ziweze kuikopesha sekta binafsi kwa riba isiyozidi asilimia 10 kwa mwaka.

Aidha, mbali na hilo BoT imelegeza masharti ya kusajili mawakala wa benki kwa kuondoa sharti la uzoefu wa kufanya biashara kwa angalau miezi 18 kwa waombaji wa biashara ya wakala wa benki, na sasa mwombaji atatakiwa kuwa na kitambulisho cha Taifa au namba ya kitambulisho cha Taifa tu.

Pia Benki Kuu imepunguza kiwango cha mtaji kinachotakiwa kuwekwa na benki za biashara ili kuweza kutoa mikopo, lengo likiwa ni kuziwezesha benki kutoa mikopo kwa urahisi.

Prof. Luoga amezisihi benki hizo kutoa mikopo zaidi kwa wakulima kwani ndiyo sekta inayogusa Watanzania wengi zaidi.