Milioni 600 kumaliza kero ya maji Mnyangamala

0
298

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amemuagiza Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo kutoa fedha za mfuko wa dharura shilingi milioni 200 kwa ajili ya kusambaza maji kwenye Kijiji cha Mnyangamala jimbo la Mchinga mkoani Lindi, ambacho kimekuwa na changamoto ya ukosefu wa huduma ya maji safi na salama kwa kipindi kirefu.

Aweso ametoa agizo hilo mara baada ya kufanya ziara kwenye jimbo hilo ambapo anasema mradi wa kusambaza maji kijijini hapo utagharimu milioni 600 lakini kwa kuanzia watatoa kiasi hicho cha milioni 200 ili shuguli ziweze kuanza haraka mwanzoni mwa mwezi Agosti.

Wananchi wa eneo hilo wamesema kwamba kwenye Kijiji hicho adha ya maji inawalazimu kutembea umbali wa zaidi ya kilomita tano kufuata huduma ya maji na kupitia changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na usalama wao.

Waziri Aweso amefanya ziara ya kikazi Wilaya ya Lindi akiitikia wito wa Mbunge wa Jimbo hilo Salma Kikwete.