Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameitaka kampuni ya China Railway 15 Bureau Group Corporation ya nchini China inayojenga barabara ya kutoka Ruangwa hadi Nanganga mkoani Lindi, kuongeza kasi ili kukamilisha ujenzi huo kwa wakati.
Waziri Mkuu Majaliwa ameyasema hayo alipokutana na kufanya mazungumzo na uongozi wa kampuni hiyo katika kijiji cha Namahema wilayani Ruangwa.
Amesema barabara hiyo ni muhimu kwa ajili ya usafirishaji wa abiria pamoja na mizigo, hivyo ni muhimu ujenzi wake ukakamilika kwa wakati.
Ujenzi wa barabara hiyo ya kutoka Ruangwa hadi Nanganga yenye urefu wa kilomita 53.2 unatarajiwa kugharimu shilingi bilioni 59.28 hadi kukamilika kwake, huku ujenzi huo ukipangwa kukamilika mwezi Novemba mwaka 2022.
Kwa upande wake, Meneja Mkazi wa kampuni ya China Railway 15 Bureau Group Corporation, Su Jinlan amemuhakikishia Waziri Mkuu Majaliwa kuwa wataongeza kasi ya ujenzi wa barabara hiyo na kwamba utakamilika kwa wakati.
Hadi sasa ujenzi huo umefikia asilimia 18.