Mbowe afikishwa mahakamani Kisutu

0
263

Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mkoani Dar es Salaa, akikabiliwa na mashtaka mawili likiwemo la kula njama ya kutenda kosa na kutoa fedha kwa ajili ya kufadhili shughuli za ugaidi.

Mbowe amefikishwa katika mahakama hiyo na kusomewa Mashtaka yake na Wakili wa Serikali Mwandamizi wa mahakama hiyo Ester Martin akisaidiana na Tulimanyw Majigo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Thomas Simba.

Katika shtaka la kwanza inadaiwa kuwa mshtakiwa huyo alitenda hilo kati Mei na Agosti 2020 katika hoteli ya Aishi iliyoko mkoani Kilimanjaro.

Katika shtaka la pili, mshtakiwa huyo anadaiwa kutoa fedha kwa ajili ya kufadhili shughuli za ugaidi, kosa ambalo anadaiwa kulitenda katika tarehe tofauti mwezi Mei na Agosti mwaka 2020 katika eneo lilipotajwa hapo awali.

Hata hivyo mshtakiwa huyo ambaye anakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 63 iliyofunguliwa mwezi mwezi Agosti mwaka 2020, hakuruhusiwa kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi

Aidha Wakili Martin amedai upelelezi umekamilika na kwamba upande wa mashtaka unaandaa nyaraka kwa ajili ya kupeleka mahakma kuu.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Agosti 5 mwaka huu kwa ajili kutajwa.

Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Freeman Mbowe, leo amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mkoani Dar es Salaam na kusomewa mashtaka yanayomkabili.

Wiki iliyopita Jeshi la Polisi nchini lilithibitisha kumshikilia Mbowe kutokana na tuhuma mbalimbali ikiwamo ugaidi na kwamba wanamshikilia ili kufanya uchunguzi wa vitendo anavyodaiwa kuvifanya ikiwa ni pamoja na uvunjifu wa amani.

Habari zaidi zinaeleza kuwa, mara baada ya kusomewa mashtaka, Mbowe amepelekwa katika gereza la Segerea baada  ya kukosa dhamana.