Majaliwa ataka taasisi za serikali ziache kutumia mkaa

0
1958

Waziri Mkuu  Kassim Majaliwa ameziagiza Wizara, mashirika na taasisi zote za Serikali na binafsi zianze kutumia nishati mbadala ili kuondoa kabisa matumizi ya kuni na mkaa.

Ametoa agizo hilo leo (Alhamisi, Mei 31, 2018) wakati akizungumza na mamia ya wananchi na viongozi wa mkoa wa Dar es Salaam walioshiriki uzinduzi wa maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam. Kaulimbiu ya mwaka huu ni: “Mkaa ni Gharama: Tumia Nishati Mbadala.”

Amesema teknolojia bora ya uzalishaji wa mkaa mbadala ambayo ameiona kwenye maonesho hayo, ikuzwe na kusambazwa kote nchini ili kuwawezesha wananchi walio wengi waachane na matumizi ya mkaa wa kawaida na badala yake watumie mkaa-mbadala kwa lengo la kuhifadhi misitu na kupunguza uharibifu wa mazingira.

Waziri Mkuu ameagiza pia kuwa vibali vya ujenzi wa majengo makubwa na taasisi kama shule, vyuo, hospitali navyo pia vianze kutolewa kwa kuzingatia ufungaji wa mifumo ya nishati ya gesi kwa ajili ya matumizi ya kupikia ili kurahisisha upatikanaji na matumizi ya nishati mbadala katika taasisi na majengo makubwa.

“Wahandisi na wachoraji ramani za majengo waweke njia za kupitisha gesi kwenye michoro yao ili ujenzi wa nyumba na majengo haya ukikamilika, watumiaji waweze kutumia teknolojia hiyo,” amesema.

Wakati huohuo, Waziri Mkuu amesema Mkoa wa Dar es Salaam ni lazima ubadilike na uachane na matumizi ya mkaa. Kwa mujibu wa takwimu zilizopo, mkoa huo unatumia tani 500,000 za mkaa kwa mwaka.

“Viongozi wa mkoa na wilaya ondokeni hapa na hili kama ajenda ya mkoa wa Dar es Salaam, mkaifanyie kazi na Wizara pia ifuatilie mmetekeleza kwa kiasi gani. Jitihada zilizofanywa na Jiji la Dar es Salaam kupitia kwa Mstahiki Meya, za kuanza kuwapa mtaji wajasiriamali hawa wanaotengeneza teknolojia mpya ni lazima ziigwe na nyie kwenye Manispaa zenu.”