UVIKO19: Serikali yaagiza ibada zisizidi saa mbili

0
422

Kutokana na mwenendo wa ugonjwa wa corona (UVIKO-19) nchini, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeagiza ibada kufanyika kwa muda usiozidi saa mbili, ili kuepusha watu kukaa sehemu moja kwa muda mrefu.

Agizo hilo limetolewa leo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Prof. Abel Makubi wakati akitangaza mwongozo wa kudhibiti maambukizi ya UVIKO19 katika maeneo yenye misongamano bila kuathiri shughuli za kiuchumi.

Aidha, ameagiza nyumba za ibada kuweka vifaa vya kunawia mikono, waumini wavae barakoa, wakae umbali unaozidi mita moja kutoka mtu mmoja hadi mwingine pande zote na utaratibu za kufanya usafi, utakasaji wa viti, meza na maeneo wanapokaa kabla na baada ya ibada ufanyike na kuepuka huduma zinazohusu kugusana.

Kwa upande mwingine serikali inakusudia kuanza utaratibu wa kufanya kipimo cha haraka cha UVIKO19 kwa mahabusu wote wanaofikishwa gerezani kwa mara ya kwanza kubaini kama wa maambukizi ama la.

Ndugu mmoja tu ndiye ataruhusiwa kumtembelea mfungwa, kumuona mahabusu katika siku iliyotengwa na kuhakikisha wafungwa na ndugu wote wanavaa barakoa na wanakuwa umbali wa mita moja kati ya mtu na mtu.

Katika vyombo vya usafiri wizara imeagiza vyombo vya ulinzi na usalama vihakikishe magari ya usafiri wa umma wanapakia abiria kulingana na idadi ya viti pasipo kusimama. Kwa magari maalumu yenye nafasi kubwa kama mwendokasi, inapolazimika kusimama basi kila abairia avae barakoa na kuachiana angalau umbali wa nusu mita.