Mkandarasi aliyechelewesha kazi aonywa

0
188

Naibu Waziri wa ujenzi na uchukuzi Mwita Waitara ameeleza kutoridhishwa na kasi ya ujenzi wa kipande cha barabara chenye urefu wa mita 800 katika barabara ya Makanya – Suji, unaotekelezwa na mkandarasi kutoka kampuni ya Bona and Hubert Engineering.

Kauli hiyo ya Naibu Waziri Waitara imekuja baada ya kutembelea ujenzi wa barabara hiyo na kukuta mkandarasi hajakamilisha, licha ya muda wa mkataba kuisha mwezi Januari mwaka huu.

“Hatutaongeza muda tena kwa sababu hakuna fedha za kulipa na hakuna malipo ya ziada, na iwapo hamtamaliza kwa kipindi cha wiki tatu au mwezi nyie mtaanza kukatwa” amesema Naibu Waziri Waitara

Amesema iwapo hatakamilisha mradi huo kwa wakati, Serikali itamfukuza na haitampa tena kazi yoyote ya ujenzi hapa nchini.

Akitoa taarifa ya ujenzi wa mradi huo Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) mkoa wa Kilimanjaro mhandisi Motta Kyando amesema, mkandarasi huyo aliomba kuongezewa muda wa ujenzi lakini hawakuridhishwa na sababu alizozitoa za kuongezewa muda.

Mhandisi wa mradi huo kutoka kampuni ya Bona and Hubert Engineering, Patrick Bruno amemuomba Naibu Waziri kumpa muda wa wiki tatu ili aweze kukamilisha ujenzi huo, kwani tayari vitu vinavyohitajika katika ujenzi wameishavikamilisha.