Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango ameagiza wizara ya fedha kurejesha kiasi cha shilingi milioni 187.7, zilizochukuliwa na mfuko mkuu wa serikali wakati wa kufunga mwaka wa fedha 2019/2020 ili zitumike katika kukamilisha miundombinu mingine ya hospitali ya wilaya ya Kakonko.
Dkt. Mpango ameagiza fedha zinazoletwa katika mradi huo kuhakikisha zinatumika vizuri na thamani ya fedha ilingane na matokeo.
Akizungumza na wananchi waliojitokeza katika uwekaji wa jiwe la msingi wa hospitali hiyo Makamu wa Rais amewahimiza wananchi wa Kakonko kuendelea kutunza mazingira kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo. Amewahakikishia kwamba serikali ya awamu ya sita iataendelea kuboresha huduma za jamii katika wilaya hiyo na kutekeleza ahadi zilizoahidiwa katika ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2020.
Pia Dkt. Mpango amepokea changamoto ya vijana wa eneo la Kakonko kushindwa kupata ajira katika mradi wa ujenzi wa barabara licha ya kwamba mradi huo unatekelezwa katika maeneo yao. Dkt. Mpango amesema serikali imeshatoa mwongozo kwa wakandarasi kuzingatia ajira kwa wazawa na kumuagiza Naibu Waziri wa Ujenzi Mhandisi Godfrey Kasekenya kulifuatilia suala hilo na kupata ufumbuzi.
Aidha Makamu wa Rais ameweka jiwe la msingi Hospitali ya wilaya ya Kakonko iliyoanza kwa ujenzi wa majengo saba yanayogharimu shilingi Bilioni 1.8 na kutarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi wa tisa mwaka 2021.