Kusaya wa DCEA atembelea TBC

0
268

Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Nchini (DCEA) Gerald Kusaya amesisitiza ushirikiano baina ya mamlaka hiyo na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) katika kutoa elimu ya kupiga vita matumizi ya dawa za kulevya.

Kamishna Jenerali Kusaya amesema hayo mkoani Dar es Salaam wakati wa ziara yake ya kutembelea ofisi za TBC, ziara iliyokuwa na lengo la kujionea namna Idara mbalimbali za shirika hilo zinavyotekeleza majukumu yake.

Amesema elimu ya kupiga vita matumizi ya dawa za kulevya hasa kwa vijana ilitalisaidia kundi hilo kupunguza matumizi ya dawa za kulevya ama kuachana kabisa na dawa hizo.

Kamishna Jenerali huyo wa DCEA pia ameipongeza TBC kwa kufanya mageuzi makubwa katika upashanaji habari ikiwa ni pamoja na kuwa na vifaa na kujenga studio za kisasa kwa ajili ya kurushia matangazo.

Ziara ya Kusaya akiwa na mwenyeji wake Mkurugenzi Mkuu wa TBC Dkt. Ayub Rioba Chacha, ilianzia katika ofisi za TBC zilizopo barabara ya Pugu na baadae katika ofisi za TBC zilizopo Mikocheni.