Tanzania yapokea ujumbe wa U.A.E

Ushirikiano Kimataifa

0
174

Umoja wa  Falme za Kiarabu (U.A.E) umeahidi kuendelea kushirikiana na Tanzania katika nyanja mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuunga mkono usawa wa kijinsia na haki za Wanawake.

Ahadi hiyo imetolewa na Mjumbe maalum wa Mfalme wa U.A.E Sheikh Shakhboot Bin Nahyan Al Nahyan alipokutana na kufanya mazungumzo na Rais Samia Suluhu Hassan Ikulu jijini Dar es Salaam.
 
Sheikh Al Nahyan amemshukuru Rais Samia kwa kuendeleza ushirikiano na nchi za Falme za Kiarabu, na kumkabidhi barua yenye ujumbe maalum kutoka kwa Mfalme wa U.A.E  Sheikh Mohamed Bin Zayed Al Nahyan.

 Aidha, Sheikh Nahyan amesema U.A.E inaunga mkono jitihada za Tanzania za kupambana na corona, ambapo amesema Umoja wa Falme za Kiarabu upo tayari kuipatia Tanzania chanjo ya ugonjwa huo.
 
Kwa upande wake Rais Samia Suluhu Hassan ameushukuru Umoja wa Falme za Kiarabu kwa kuendeleza ushirikiano na Tanzania, na kumuahidi Mjumbe huyo maalum kuwa Serikali itaendeleza ushirikiano huo kwa  manufaa ya pande zote mbili.
 
Amesema U.A.E ni mbia muhimu katika maendeleo ya Tanzania kwa sababu imesaidia kuboresha miundombinu hasa ya barabara.
 
Rais Samia Suluhu Hassan pia ameshukuru kupokea mwaliko wa kuhudhuria Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dubai (Dubai Expo) yanayotarajiwa kufanyika mwezi Machi mwaka 2022.