Wasimamizi wa miradi watakiwa kujitathmini

0
186

Mkuu wa mkoa wa Mara, Ally Hapi amewataka Wasimamizi wa miradi inayotekelezwa katika ofisi yake kujitathmini kama kweli wanaweza kusimamia miradi hiyo.

Hapi ameyasema hayo mara baada ya kukagua miradi ya ujenzi wa nyumba za Viongozi wa Serikali, ambapo amebaini usimamizi mbovu katika miradi hiyo hali inayoiingizia hasara Serikali.

Amesema mapungufu yaliyoonekana katika miradi hiyo ni makubwa, huku wasimamizi hao wakikosa uaminifu katika utekelezaji wa miradi hiyo kutokana na gharama za miradi kukosa uhalisia wa thamani ya fedha iliyotumika.

Mkuu huyo mkoa wa Mara amesema mbali na usimamizi mbovu wa miradi hiyo, lakini pia wameshindwa kutumia vizuri utaratibu wa Force Akaunti kwa kutumia fundi mmoja katika jengo, ilihali wana uwezo wa kuweka mafundi wengi ili kuongeza kasi ya utekelezaji wa mradi.

Hapi amewataka Wasimamizi hao kuwa makini pamoja na kuwa waadilifu na wachapakazi, vinginevyo hatua kali zitachukuliwa dhidi yao ikiwa ni pamoja na kuenguliwa katika nafasi zao.