Waziri wa Maji Jumaa Aweso ameivunja kampuni ya Kiliwater iliyokuwa na kazi ya kusimamia na kuendesha miradi ya maji wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro, na kutangaza rasmi kuanza kwa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Rombo.
Waziri Aweso amefikia uamuzi huo baada ya kuona tangu kampuni hiyo ianzishwe miaka 25 iliyopita, imeshindwa kukidhi matakwa ya usambazaji wa huduma ya maji safi na salama kwa Wananchi.
“Haiwezekani kwa kipindi chote hicho uongozi wa kampuni hii ushindwe kuwafikishia Wananchi huduma ya maji safi na salama na kuwaacha wakiendelea kuteseka.” amesema Waziri Aweso
Amemteua Martin kinabo kuwa Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka hiyo ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Rombo na kumtaka ahakikishe anasimamia mapato pamoja na kuwatambua wateja wa kampuni hiyo.
Awali akisoma taarifa ya kampuni ya Kiliwater kwa Waziri Aweso, Meneja Mkuu wa kampuni hiyo Prosper Kessy alisema kuwa, changamoto kubwa waliyokuwa wakikabiliana nayo ni upotevu wa maji ambapo asilimia 60 ya maji yanayokusanywa hupotea.
Tayari Serikali imetoa shilingi bilioni 10 kwa ajili ya kumaliza tatizo la maji wilayani Rombo, kwa kuanzisha vyanzo vipya na kuboresha vile vilivyopo.