Watumishi 9 wasimamishwa kazi JNIA

0
325

Watumishi tisa wa Kitengo cha upimaji wa COVID-19 kwa wasafiri katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam wasimamishwa kazi.

Agizo hilo limetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Prof. Abel Makubi alipofanya ziara uwanjani hapo kukagua utekelezaji wa maelekezo aliyoyatoa juzi.

Prof. Makubi amesema hakufurahishwa na kitendo cha utovu wa nidhamu kilichofanywa na watumishi cha kutokufika kazini bila kutoa taarifa rasmi kwa uongozi.

“Jana watumishi wanane hawakufika na leo mmoja bila kutoa sababu ya msingi, jumla wanakuwa tisa. Hii imenisikitisha sana kwa baadhi ya viongozi kushindwa kuchukua hatua zinazostahili na kulindana kwa kuficha uozo,” ameeleza Makubi.

“Huu ni utovu wa nidhamu wa hali ya juu ambapo mtumishi anaamua kuacha kuja kazini na kusababisha usumbufu kwa wenzake na abiria ambao wanakuja hapa kwa sababu yeye ‘gap’ yake haijawa ‘covered’ na mtu yeyote,” amesisitiza na kuongeza kuwa serikali haiwezi kuvumilia watumishi wasio na nidhamu na wanaodharau majukumu wanayopewa.

Amehidi kupeleka watumishi wengine kushika nafasi zao ili kutoathiri shughuli za upimaji na kuwataka watumishi wote wa afya kutanguliza uzalendo wa hali ya juu katika utendaji wa kazi zao na kwa kujituma.