Ugomvi wa familia wasababisha kifo

0
204

John Wilbard, mkazi wa kijiji cha Chala wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro anashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani humo kwa tuhuma za kumuua mtoto wake Amedeus Kavishe.

Kamanda wa polisi wa mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amesema Wilbard anadaiwa kufanya mauaji hayo wakati wa ugomvi wa kifamilia.

Amesema marehemu amefariki dunia wakati akiwahishwa hospitalini baada ya kukatwa sehemu ya shingoni na kitu chenye ncha kali.

Kamanda Maigwa amesema marehemu Amedeus alikuwa akigombana na mke wake, ndipo baba mzazi alikwenda kuamua ugomvi huo.

Amesema marehemu alimtukana baba yake kisha kumpiga na jiwe kichwani, kitendo kilichosabahisha baba yake kupandwa na hasira na kisha kuchukua panga kumkata mwanae shingoni.

Mwili wa marehemu Amedeus umehifadhiwa katika hospitali ya Ngoyoni.