Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Doroth Gwajima amelitaka Baraza la Mashirika yasiyokuwa ya kiserikali (NaCONGO) kufanya kazi kwa weledi, uadilifu na uzalendo pamoja na kuzingatia Sheria, kanuni na miongozo iliyopo ili kukidhi matarajio ya waliowachagua.
Dkt. Gwajima ameyasema hayo jijini Dodoma wakati akipokea taarifa na kuzindua Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyokuwa yakiserikali (NaCONGO).
Aidha Waziri Gwajima amelitaka Baraza hilo kufanya kazi weledi,uadilifu na uzalendo. Amesema Baraza hilo lilifanya uchaguzi mwaka 2016 ambapo mara baada ya hapo waliokuwa viongozi waligoma kufanya uchaguzi.
“Nitoe shukrani zangu za dhati kwa kusimamia zoezi hili,Tunautambua umuhimu wenu na hivyo tunawapongeza sana,”amesema Dkt. Gwajima.
Waziri Gwajima amemtaka Mwenyekiti wa Baraza hilo, Lilian Badi kusimamia vyema NaCONGO ili mambo yaende vizuri.
“Baraza hili ni zito. simama kwenye nafasi yako, kwenye pesa mayuda hawakosekani,” amesisitiza Waziri Gwajima
Kwa upande wake, Mwenyekiti mpya wa NaCONGO, Lilian Badi ameahidi kufanya kazi kisayansi na kwa uadilifu mkubwa ili kuirudisha NaCONGO katika ubora wake.
Amesema watakuwa mabalozi wa msajili katika Wilaya kwa kuhakikisha NGO’s zinafuata taratibu na sheria katika kujiendesha.