Mazishi ya mhubiri maarufu duniani Temitope Balogun Joshua maarufu TB Joshua wa nchini Nigeria yamefanyika leo nchini humo.
TB Joshua alifariki dunia Juni 5 mwaka huu nchini Nigeria akiwa na umri wa miaka 57.
Mazishi ya TB Joshua yamefanyika ndani ya kanisa lake la Synagogue Church of All Nations (SCOAN) mjini Lagos.
Kabla ya mazishi hayo, Ibada ya kuaga mwili wa mhubiri huyo maarufu ilifanyika kanisani hapo ambapo pia maelfu ya waombolezaji walijitokeza kuaga mwili huo.
Taratibu za mazishi ya TB Joshua zilianza Jumatatu wiki hii, ikianza na misa katika kanisa hilo na siku ya Jumanne waombolezaji walianza kutoa heshima zao za mwisho.
TB Joshua alijipatia umaarufu kutokana na huduma yake ya maombi ambapo pia alitumia huduma hiyo kuwaponya watu mbalimbali, na hivyo kuifanya huduma hiyo kuwa maarufu duniani.