Tanzania kushirikiana na UNEP kutunza mazingira

0
303

Rais Samia Suluhu Hassan ameahidi kushirikiana na Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) katika mipango thabiti ya utunzaji na uhifadhi wa mazingira nchini.

Rais Samia Suluhu Hassan ametoa kauli hiyo Ikulu mkoani Dodoma alipokutana na kufanya mazungumzo na Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP Joyce Msuya.

Ameiomba UNEP kuhakikisha mpango wa Umoja wa Mataifa wa miaka mitano wanaouandaa uwe endelevu na wenye kuleta tija katika kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi hapa nchini.

Rais Samia Suluhu Hassan amesema Serikali inaendelea na jitihada mbalimbali za kukabiliana na uharibifu wa mazingira ikiwa ni pamoja na kuwawekea mazingira bora Wananchi katika shughuli zao za maendeleo ili wasizidi kuharibu mazingira.

Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi Mtendaji huyo wa UNEP Joyce Msuya amesema shirika hilo kwa kushirikiana na Umoja wa Mataifa wako tayari kuunga mkono jitihada mbalimbali zinazofanywa na Tanzania katika maendeleo na mipango yake ya kutunza na kuhifadhi mazingira.

Amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake anazochukua kukabiliana na Corona, ambapo amesema Umoja wa Mataifa uko tayari kuunga mkono jitihada hizo.

Mazungumzo hayo pia yamehudhuriwa na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) Christine Musisi ambaye amesema kuwa kupitia mpango mkakati wa miaka mitano wanaouandaa, watazingatia mpango wa maendeleo wa tatu wa miaka mitano wa Tanzania.