Mkuranga wahimizwa kusomesha Watoto

0
161

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega, amewahimiza Wananchi wa wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani kusomesha watoto wao, ili kupata elimu itakayowasaidia kukabiliana na changamoto za maisha.

Ulega ameyasema hayo wakati wa mkutano wa hadhara katika kijiji cha Mihekela akiwa kwenye ziara ya kibunge jimboni kwake Mkuranga.

Aidha Naibu Waziri Ulega amesema Serikali imeendelea kutilia mkazo suala la utoaji elimu kwa Watanzania, ili kwenda na kasi ya ukuaji wa uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

“Niwaombe ndugu zangu tusiache kupeleka watoto shuleni wakapate elimu maana ndio itawakomboa maana Rais wetu Samia Suluhu Hassan kupitia Serikali yetu ameendelea kuboresha upatikanaji wa elimu bora kwa watoto wetu, hivyo ni lazima kila mtu kutumia fursa hiyo.” amesema Naibu Waziri Ulega.

Amesema katika siku 100 za uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, tayari fedha nyingi zimeishapelekwa Mkuranga kwa ajili ya maendeleo ikiwemo elimu, afya na barabara.

Akiendelea na ziara ya kibunge jimboni kwake, Ulega amechangia shughuli za maendeleo ambapo katika kijiji cha Mihekela amechangia fedha kwa ajili ya kuanzishwa kwa kikundi cha ujasiriamali na kukabidhi bati 90 na shilingi milioni moja kwa ajili ya kuezeka majengo ya shule ya msingi Mihekela.