Zuma ajisalimisha, aanza kutumia kifungo gerezani

0
248

Polisi nchini Afrika kusini imethibitisha kwamba aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Jacob Zuma amejisalimisha mwenyewe Polisi.

Hatua hiyo ya Zuma imekuja ikiwa imepita wiki moja tangu alipokutwa na hatia ya kuidharau Mahakama katika kesi yake ya ufisadi na kuhukumiwa kifungo cha miezi 15 gerezani.

Usiku wa kuamkia leo umekuwa ni wa kwanza gerezani kwa Jacob Zuma, baada ya kujisalimisha mwenyewe kwa mamlaka husika jana (Julai 7).

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewana Polisi wa Afrika ya Kusini Rais huyo mstaafu ameamua kutii agizo la ?mahakama na kukubali kutumikia kifungo chake

Baada ya kufikia makubaliano ya kujisalimisha kwake na ujumbe wa Polisi uliofika nyumbani kwake mapema jana, Zuma akiwa na walinzi wake ameenda katika gereza lililokaribu na nyumbani kwake katika jimbo la KwaZulu Natal.

Baadhi ya wafuasi wake waliokuwa wamekusanyika nje ya nyumba yake walielezea kutofurahishwa na kiongozi wao kuhukumiwa kifungo gerezani.

Zuma mwenye miaka 79 amehukumiwa kifungo cha miezi 15 gerezani, wiki iliyopita baada ya kushindwa kufika mahakamani kusikiliza kesi ya rushwa iliyokuwa ikimkabili.

Hukumu dhidi ya Zuma ambayo ni ya kwanza dhidi ya Rais wa nchi, ilizua mtafaruku wa kisheria nchini Afrika kusini, huku muda wa mwisho uliowekwa wa kujisalimisha ama kukamatwa kwake ukiwa ni jana usiku.