Shilingi bilioni 1.4 kujenga barabara Same

0
174

Wakazi wa kata ya Vunta wilaya ys Same mkoani Kilimanjaro, wamemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kusikia kilio chao cha ubovu wa barabara kwa kuwatengea shilingi bilioni 1.4 katika jimbo la Same Mashariki ili kutatua changamoto hiyo.

Wakizungumzia siku 100 za Rais Samia Suluhu Hassan tangu aingie madarakani, Wakazi hao wamesema ni muda mrefu barabara hizo ambazo ni za milimani zimesahaulika kutengewa fedha, lakini kwa kipindi cha uongozi wa awamu ya Sita wameweza kutengewa fedha na ujenzi unaendelea katika baadhi ya barabara.

Wamesema ubovu wa barabara sio tu umekuwa ukikwamisha shughuli za maendeleo, lakini pia wamekuwa wakitumia gharama kubwa kwenye usafiri kwa kulipa shilingi elfu 30 kushuka na kupanda kwa kutumia pikipiki.

Kwa upande wake, Mbunge wa jimbo la Same Mashariki Anne Kilango Malecela amesema changamoto kubwa ya wakazi wa maeneo hayo ni kushindwa kusafirisha mazao yao hasa tangawizi kutoka mashambani kwenda kuuza sokoni kutokana na ubovu wa barabara.

Meneja wa Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) wilayani Same Mhandisi felician Msangi amesema hali ya barabara katika jimbo la Same Mashariki hairidhishi, na tayari wakala huo umepokea shilingi milioni 400 kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Hedaru-Vunta-Mamba yenye urefu wa kilomita 42 kwa kiwango cha changarawe.