FITI kuhamishiwa Mafinga

0
174

Wizara ya Maliasili na Utalii imesema iko katika mchakato wa kukihamisha chuo cha Viwanda vya Misitu (FITI) kilichopo mjini Moshi mkoani Kilimanjaro kuhamia Mafinga mkoani Iringa, ili kukiwezesha kufanya kazi kwa ufanisi zaidi kutokana na uwepo malighafi za misitu katika eneo hilo.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Damas Ndumbaro wakati alipotembelea chuo hicho na kuzungumza na uongozi, na kuongeza kuwa kutokana na uwepo wa misitu huko Mafinga hakutakuwa na haja ya kutumia gharama za kusafirisha magogo kwa ajili ya matumizi ya kutengeneza bidhaa mbalimbali zitokanazo na misitu chuoni hapo.

“Mafinga ndio sehemu yenye viwanda vingi vya mbao vya watu binafsi, na hiyo itasaidia Wanafunzi kufanya mafunzo kwa vitendo katika viwanda hivyo na tunazo hekta 120 za Serikali ambazo sio za kununua na kwamba suala la kuhama haliepukiki.” amesema Waziri Ndumbaro

Amebainisha kuwa chuo cha FITI Moshi hakitafungwa bali kitakuwa ni tawi, na kwamba Mafinga kutajengwa majengo ya kisasa na mashine za kisasa ambazo zitawezesha utendaji kazi wa chuo hicho kiurahisi kuliko ilivyo sasa Moshi.