Rais Samia: Mfugale ametuachia simanzi

0
358

Rais Samia Suluhu Hassan amesema kuwa kifo cha aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Patrick Mfugale kimeacha simanzi na pengo kubwa kwa familia, Serikali na Taifa kwa ujumla.

Rais ameeleza hilo kwa huzu alipowaongoza viongozi mbalimbali na waombolezaji kuaga mwili Mhandisi Mfugale katika viwanja vya Karimjee Jijini Dar es Salaam.

Amesema Serikali imepoteza mtumishi na kiongozi mwadilifu, makini, shupavu na mchapakazi hodari na taifa limepoteza mhandisi mahiri na mzalendo wa kweli ambaye daima alikuwa tayari kuitumikia nchi kwa moyo wake wote.

Alikuwa mtumishi wa umma kwa takribani miaka 45, tangu mwaka 1977 ambapo ameongoza TANROADS kwa takribani miaka 12 tangu mwaka 2009.

Mhandisi Mfugale atakumbukwa kwa kubuni na kusimamia ujenzi wa Daraja la Umoja (Mtambaswala) linalounganisha Tanzania na Msumbiji, Daraja la Nyerere (Kigamboni), Daraja la Mkapa katika Mto Rufiji, Daraja la Kikwete katika Mto Malagarasi, Daraja la Magufuli katika Mto Kilombero, Daraja la Mfugale (TAZARA), Daraja la Kijazi (Ubungo), Daraja la Tanzanite (Selander), Daraja la Kigongo – Busisi (JPM), na Miradi mingi ya kimakakati.