Dkt. Mpango afurahia utunzaji mazingira Paris

0
191


Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango amekutana na kufanya mazungumzo na mwenyekiti wa kundi la Maseneta wa Kifaransa marafiki wa Tanzania, Ronan Dantec.



Mazungumzo hayo yamefanyika katika jengo la Bunge la Seneti huko Paris nchini Ufaransa, ambapo wamejadili umuhimu wa kuhifadhi mazingira ili kupunguza hewa ya ukaa duniani.

Wakati wa mazungumzo hayo, Dkt. Mpango ameelezea kufurahishwa na namna uhifadhi wa mazingira unavyofanyika nchini Ufaransa ikiwemo katika jiji la Paris licha ya ukongwe wa mji huo.

Dkt. Mpango amemuhakikishia Seneta Dantec kuwa Tanzania ipo tayari kushirikiana na Ufaransa katika uhifadhi wa mazingira, na amewakaribisha Maseneta rafiki wa Tanzania katika kutekeleza jambo hilo kwa pamoja.

Akiwa katika jengo hilo la Bunge la Seneti huko Paris, Makamu wa Rais pia ametembelea maktaba iliyopo katika jengo hilo na kujionea historia mbalimbali zilivyohifadhiwa.

Makamu wa Rais yuko nchini Ufaransa kuhudhuria Jukwaa la Kizazi Chenye Usawa, ambalo lina lengo la kuchagiza haki za usawa wa kijinsia kama ilivyokubaliwa katika mkutano wa Beijing wa mwaka 1995.