Bodi ya Utalii yahamasisha Utalii wa Mikutano

0
290

Katika kuhakikisha sekta ya utalii inaendelea kukua, Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), imeanza kuhamasisha utalii wa mikutano ambao unawakutanisha wadau wengi kwa wakati mmoja.

Kuhakikisha miundombinu ya utalii wa mikutano inakidhi vigezo, bodi hiyo imetembelea baadhi ya hoteli zilizopo jijini Dodoma kujionea hali ya mazingira ya hoteli hizo na kuona kama zimejiandaa kupokea wageni mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi.

Akizungumza na TBC, Mkuu wa Masoko wa hoteli na ukumbi wa mikutano wa St. Gaspar, Geofrey Msaga ameipongeza bodi hiyo kwa kuona fursa nyingine ya utalii na kufungua milango kwa wadau ndani na nje ya nchi ya kuandaa mikutano ambayo itasaidia wadau hao kutembelea maeneo mengine ya kitalii yaliyopo eneo hilo.

“Niipongeze bodi ya utalii kwa kuliona hili na sisi kama wadau wa sekta hii tunaahidi kutoa ushirikiano kwa wote watakaotembelea maeneo mbalimbali ya Dodoma”, amesema Geofrey.

Utalii wa mikutano unatoa fursa kwa wadau wanaoshiriki mikutano hiyo, kupata nafasi ya kutembelea maeneo mengine ya kitalii yaliyopo karibu kujionea mazuri ndani ya jiji la Dodoma la maeneo jirani.