Rais Samia aachwe aongoze kwa namna yake

0
295

Wananchi wametakiwa kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan katika kutimiza majukumu yake na kumruhusu aongoze kwa namna yake ya kipekee.

Hayo yamesemwa na viongozi wa dini za Kikristo na Kiislamu waliojumuika pamoja kwenye “Kongamano la Kumuombea na Kumshukuru Mungu kwa Siku 100 za Rais Samia Suluhu Hassan Madarakani” mkoani Dar es Salaam.

Katika kongamano hilo viongozi hao wamekumbusha kuhusu nafasi kubwa ya mwanamke na uwezo Mungu alioweka ndani ya mwanamke kwa kutumia mifano iliyomo kwenye vitabu vitakatifu vya Quran na Biblia.

Sheikh Kipozeo ameongeza kuwa wanawake wana wanaweza kushika nafasi kubwa za uongozi na kuzitendea haki kwa kusema “Kuna wanawake wana akili kuliko wanaume.”

Aidha, Askofu Zachary Kakobe ameelezea baadhi ya minong’ono iliyopo kwenye jamii kuhusu utofauti wa uongozi wa Rais wa sasa na Hayati, Dkt. John Magufuli pamoja na kuwa wengine wanahisi hawakumchagua Rais Samia Suluhu Hassan na kusema wote waliomchagua Hayati Magufuli walimchagua Rais Samia Suluhu Hassan kwani waliwania pamoja na mwananchi alipiga kura akijua hili.

“Rais Samia Suluhu Hassan, wewe upo hapo kama Rais, hujawekwa hapo kuwa muigizaji wala msanii. Kwasababu hii, tuongoze kwa staili yako mwenyewe.

“Kazi ni ileile… nia ni ileile,ilani ni ileile. Kwahiyo kazi inaendelea, lakini staili ya uongozi inakuwa ni tofauti,” amesema Askofu Kakobe.

Pia, Serikali imeombwa kushirikiana na viongozi wa dini lakini pia wananchi kuendelea kusali na kuikabidhi nchi mikononi mwa Mwenyezi Mungu.