Askari akutwa amefariki lindoni

0
305

Askari wa Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la kujenga Taifa – Suma JKT, Emmanuel Malya amekutwa amefariki dunia usiku wa Juni 21,2021 katika kituo cha kupoozea umeme cha Kiyungi kilichopo wilayani Moshi mkoani Kilimanjaro.

Akizungumzia tukio hilo Kamanda wa Polisi mkoa wa Kilimanjaro, Amon Kakwale amesema mwili wa askari huyo ambaye ni mlinzi katika kituo hicho ulikutwa ukiwa pamoja na silaha aina ya shotgun pembeni.

Kamanda Kakwale amesema katika eneo hilo polisi walikuta pia maganda matatu ambayo yameonesha ni kutoka katika silaha hiyo.

Amesema katika kituo hicho kulikuwa na askari wawili ambao ni walinzi, lakini hadi sasa hawajampata askari huyo wa pili na kwamba wanaendelea kumtafuta kwa mahojiano zaidi.

Kamanda Kakwale amebainisha kuwa bado uchunguzi unaendelea kujua nani amefanya mauaji hayo pamoja na kujua chanzo chake.