Malima : Tumieni madaraka yenu vizuri

0
205

Mkuu wa mkoa wa Tanga, Adam Malima amewataka wakuu wa wilaya mkoani humo kutumia vizuri madaraka yao, ili kuwaletea Wananchi maendeleo na si vinginevyo.

Malima ametoa kauli hiyo wakati akiwaapisha wakuu wapya wa wilaya za mkoa huo walioteuliwa hivi karibuni na Rais Samia Suluhu Hassan.

Amesema ni muhimu kila mmoja akatimiza majukumu yake ya kimsingi kwa kuwa kazi ya kutumikia Wananchi inahitaji ubunifu na kuvielewa vema vipaumbele vya Taifa.

“Sitegemei kuona mtu anatumia madaraka yake vibaya ikiwa ni pamoja na kuwaweka watu ndani, kuwanyanyasa na kutumia nguvu eti kisa una mamlaka. Jambo hilo silitaki katika mkoa wa Tanga, badala yake tumieni muda mwingi kuwaletea maendeleo Wananchi.” amesema Malima.

Aidha amesema uwepo wa uwekezaji wa mradi mkubwa wa bomba la mafuta ni fursa kwa Wakazi wa mkoa wa Tanga, hivyo wakuu wa wilaya wanao wajibu wa kusimamia kwa karibu na kuhakikisha Wananchi wanashiriki kikamilifu.

Mkuu huyo wa mkoa wa Tanga pia amewataka Wakuu hao wa wilaya kuimarisha zao la Mkonge katika wilaya zote zinazolima zao hilo.

Mkoa wa Tanga una jumla ya wilaya nane, ambapo wakuu wa wilaya walioapishwa ni wanne na wanne wengine wamehamishiwa mkoani humo wakitokea vituo vingine vya kazi.